Satelaiti ya Facebook ya kufikisha mtandao kasi Afrika yaharibiwa
Mwanzilishi wa kampuni ya Facebook Mark Zuckerberg amelezea kusikitishwa kwake baada ya satelaiti ambayo Facebook ingeitumia kwa mawasiliano ya kasi ya mtandao wa intaneti barani Afrika kuharibiwa. Satelaiti hiyo iliharibiwa katika mlipuko uliotokea eneo la Cape Canaveral jimbo la Florida, Marekani siku ya Alhamisi. Satelaiti hiyo kwa jina Amos-Six ilikuwa imebebwa na roketi ya Falcon Nine ambayo ililipuka ilipokuwa ikifanyiwa majaribio ya kujiandaa kwa safari ya siku ya Jumamosi. Mlipuko huo ulitokea wakati roketi hiyo ilikuwa ikijazwa mafuta na kutikiza majengo yaliyokuwa umbali wa kilomita kadha. Bw Zuckerberg, ambaye yumo ziarani Afrika, amesema "nimesikitishwa sana" kusikia kwamba satelaiti hiyo iliharibiwa. "Tutaendelea kujitolea katika lengo lengo la kufikisha huduma ya mtandao kwa kila mtu na tutatia bidii hadi kila mtu apate nafasi na manufaa ambayo yangetokana na satelaiti hii," aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook.