Mwili wa binadamu waweza kufananishwa na nyumba
inayojengwa, nyumba hujengwa kwa matofali, simenti, chokaa na malighafi
nyingine nyingi, na inahitaji ukarabati wa mara kwa mara ili iendelee kuwa
nyumba bora, nyumba iliyoachwa kukaliwa na binadamu huchakaa haraka na pengine
hubomoka kabla ya wakati wake. Mwili wa binadamu nao kama ilivyo nyumba una
mahitaji yake, unahitaji chakula bora ili uendelee kubaki katika hali ya afya
nzuri,
pia unahitaji mazoezi ya viungo ili uweze kuwa imara na wenye nguvu.
Mwili wa binadamu hata viumbe wengine(wanyama) unapokosa mazoezi hunyong’onyea
na mifumo ya mwili hushindwa kufanya kazi vizuri inavyotakiwa.
Mazoezi ya mara kwa mara au kufanya kazi zinazohusisha
matumizi ya nguvu ya mwili yanasaidia mifumo mingi ya mwili kufanya kazi
inavyotakiwa, mazoezi yatatuepusha na magonjwa ya moyo, kisukari, na hata magonjwa
mengine hayataweza kushambulia miili yetu, na ni njia nzuri ya kupunguza uzito
wa mwili uliozidi. Unapokuwa unafanya mazoezi mara mara utafaidika na mambo
yafuatayo:
Moja ni kuongeza nafasi ya kuboresha umri wa kuishi na
kuishi katika afya njema.
Pili mazoezi yanasaidia kutulinda na magonjwa ya moyo,
kiharusi na magonjwa yanayoambatana nayo kama shinikizo la damu na ongezeko au
kiwango cha juu cha lehemu katika damu. Kiwango cha juu cha lehemu katika damu
kimekuwa kisababishi cha ongezeko la shinikizo la damu na hata kuwa katika
hatari ya kupata kiharusi.
Tatu mazoezi yanatusaidia kuepukana na magonjwa ya
kansa fulani kama kansa ya tumbo, kansa ya matiti, kansa ya mapafu na kansa ya
kizazi. Hii ni kwa sababu mazoezi yanaboresha mifumo mbali mbali ya mwili na
kuwezesha mwili kutoa taka na sumu mbali mbali mwilini, pamoja na kuimarika kwa
kinga ya asili ya mwili.
Tafiti za wanasayansi zilizofanyika hivi karibuni
zinaonyesha kuwa mazoezi yanasaidia kutokupoteza uwezo wa kuona. Matatizo mengi
ya kuona hujitokeza mara nyingi kwa wazee, kwa hiyo tunaweza kuzuia hali hiyo
isijitokeze kwa kufanya mazoezi.(
kwa
mujibu wa jarida la newscientist la marekani)
Pia mazoezi yanasaidia kutukinga na kisukari aina ya
pili (ugonjwa ambao mtu anaupata ameshakuwa mkubwa na sio kwa kuzaliwa), na
kutukinga na matatizo ya mmeng’enyo ambayo yanaweza kutuletea magonjwa ya moyo
na kisukari pia.
Mazoezi yanasaidia pia kutukinga na matatizo ya
mmomonyoko wa mifupa (osteoporosis) ambayo mara nyingi hujitokeza uzeeni.
Yanaimarisha afya ya akili, yanasaidia kutuepusha na magonjwa ya kupoteza
kumbukumbu hasa kwa wazee. Pia mazoezi yanatuondolea msongo wa mawazo, woga na
mtu kuwa katika afya nzuri ya akili.
Mazoezi yanasaidia kuwa na mapafu yenye kufanya kazi
vizuri,moyo wenye afya na kuimarisha misuli ya mwili kwa ujumla. Bila kusahau
kuwa mazoezi husaidia kupata usingizi mzuri kwa afya bora.
Kwa hiyo basi kama mazoezi ya mara kwa mara na kazi
zinazohusisha matumizi ya nguvu za mwili zina faida katika afya ya miili yetu,
maisha ya ulegevu yatakuwa na matokeo ambayo ni kinyume chake.