MICHEZO: Van Gaal afukuzwa
asa ni rasmi, Manchester United wamemfukuza kazi kocha wao, Louis van
Gaal, siku mbili tu tangu alipowapatia Kombe la FA kwenye fainali
iliyopigwa dhidi ya Crystal Palace dimbani Wembley.
Van Gaal anaondoka na wasaidizi wake wote wa Kidachi kwenye benchi la
ufundi, Albert Stuivenberg, Frans Hoek na Max Reckers ambapo Jose
Mourinho ataichukua nafasi hiyo. Ikumbukwe kwamba Mourinho alikuwa
msaidizi wa Van Gaal klabuni Barcelona.
Kocha huyo wa zamani wa Timu ya Taifa ya Uholanzi, Bayern Munich,
Bercelona, Ajax na Az anaondoka kwa sababu uongozi na wamiliki wa Man
United hawaridhiki na aina ya ufundishaji wake na timu kumaliza katika
nafasi ya tano kwenye Ligi Kuu ya England.
LVG aliwasili kwenye uwanja wa mazoezi wa Carrington asubuhi ya
Jumatatu hii kama kawaida, lakini akiwa na sintofahamu juu ya hatima
yake, kisha akafuatiwa na wakili wa Chama cha Makocha wa Ligi, Paul
Gilroy QC, ambaye amefanya kazi kwa muda mrefu huko.
Baada ya Makamu Mwenyekiti Mtendaji, Ed Woodward kuwasili, walikwenda
ndani kwa kikao, ndipo akamwarifu Van Gaal kwamba hatakuwa tena kocha
wao na kwamba wameamua kumchukua Mourinho badala yake.
Mchambuzi wa utendaji wa Van Gaal aliyekuwa akimuamini sana, Max
Reckers, aliyesababisha msuguano na familia ya Manchester United,
kadhalika ameoneshwa mlango wa kutokea Old Trafford. Awali alizuiwa na
walinzi kuingia, lakini baadaye akaitwa baada ya LVG kuwasili.
Mourinho anatarajiwa kufanya mazungumzo zaidi Jumanne hii na wakuu wa
Man U kabla ya kusaini mkataba wa miaka mitatu sambamba na mshirika
wake wa siku nyingi aliyeondolewa naye Chelsea, Rui Faria na kocha wa
makipa, Silvino Louro.
Hatima ya kocha msaidizi wa sasa Man U, Ryan Giggs ipo shakani,
ikidaiwa kwamba Mourinho anajidai kwamba anataka kumbakisha kwenye
nafasi hiyo lakini raia huyo wa Wales hapendi kufanya naye kazi, kwani
aliamini ama LVG angebaki au yeye kupewa mikoba hiyo, baada ya kuwa
hapo kama mchezaji na sasa kocha msaidizi kwa miaka 29.
sc@TanzaniaSport